TAA Yaandaa Mikakati ya Kudhibiti Viashiria Hatarishi

TAA Yaandaa Mikakati ya Kudhibiti Viashiria HatarishiMAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imeanza mikakati ya kujiwekea mfumo wa viashiria hatarishi (Risk Management) kwa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wake, ambayo yameanza jana kwenye ukumbi wa mikutano wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) uliopo Kipawa jijini Dar es Salaam.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka, ambapo yanashirikisha washiriki kutoka Idara mbalimbali, Bw. Lawrence Thobias ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yatatumika kama sehemu ya kazi, hivyo washiriki wote wazingatie na kujifunza kwa bidii.

"Ninajua wote waliopo kazini wanauwezo na nyie mmechaguliwa wachache na hamuwezi kuja wote katika mafunzo haya, ila ninachowaomba mjifunze kwa bidii na mshirikishane yale mnayoyafahamu kwani wote hapa ni wazoefu ili kuleta ufanisi bora na mzuri katika Taasisi yetu," amesema Bw. Thobias.

Bw. Thobias amesema kuwa baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo TAA itatengeneza nyaraka za viashiria hatarishi kwa kutumia wataalamu watakaochaguliwa miongoni mwa washiriki, ambazo zikikubalika kwa viwango vinavyotakiwa basi itatakiwa kusimamiwa na kuendeshwa vyema na Mamlaka.

Naye Naibu Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali (Usimamizi wa Viashiria Hatarishi, Mfumo na Udhibiti wa Ndani), kutoka Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Bw. Emmanuel Subbi kutoka Ofisi ya Mkaguzi wa Hesabu, amesema wameamua kutoa mafunzo ya viashiria hatarishi (Risk Management) kwa Taasisi za Serikali ili waweze kuishauri Serikali namna ya kuzizuia na kuzidhibiti kabla ya kutokea.

Bw. Subbi amesema kila Taasisi inatakiwa kuwa na mwongozo wa viashiria hatarishi wa mwaka 2013 na pia Waraka wa Hazina namba 12 ya mwaka 2013, ambapo zote zinaonesha namna na jinsi ya kuzuia viashiria hatarishi.

"Mfumo huu una faida kubwa kwa Taasisi za Umma kwani unasaidia kuaminika na hata kupata mikopo kutoka katika Taasisi mbalimbali Duniani, pia mfumo huu utakupa nafasi nzuri ya kufanya maamuzi kwa upana ikiwa unaangalia na mfumo wako wa kazi," amesema Bw. Subbi.

Pia Bw. Subbi amesema mfumo huu utasaidia kuepuka matatizo katika ununuzi, sheria, viwango na udhibiti, ambapo miaka ijayo itapunguza kupatikana kwa hati chafu kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu (CAG), ambapo mfumo ukizingatiwa hakutakuwa na matatizo hayo kwani watagundua viashiria hatarishi kabla havijatokea na kuleta madhara.

MWISHO

Contact Us

Tel (Gen): +255 22 2842402/3
Fax: +255 22 2844495
Email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
P.O.Box 18000 Dar Es Salaam

Feedback & Enquires