Uchukuzi SC yaahidi kuendeleza ubabe SHIMIWI

TIMU ya michezo ya Sekta ya Uchukuzi (USC), imeahidi kuendeleza ubabe kwa kufanya vyema katika mashindano mbalimbali ya Watumishi wa Umma ikiwemo michezo ya Wizara, Idara na Taasisi za Serikali (SHIMIWI); Mei Mosi na mabonanza mbalimbali.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Mhandisi Dkt Leonard Chamuriho leo katika bonanza la uzinduzi wa mazoezi ya michezo ya SHIMIWI inayotarajia kufanyika Mkoani Dodoma kuanzia Septemba 25 mpaka Oktoba 3.

Mhandisi Dkt. Chamuriho amesema ana matumaini makubwa na timu ya Uchukuzi kwakuwa imekua ikileta ushindani na ushindi katika mashindano mbalimbali ambayo imekuwa ikishiriki.

"Nina imani kubwa sana na timu hii ya Uchukuzi kwa kuwa mmekuwa mkileta ushindi kila mnaposhiriki, nimefurahi pia kusikia kwamba mmeshida vikombe vinane vya ushindi wa kwanza, vikombe viwili vya ushindi wa pili na vikombe vitatu vya ushindi wa tatu na hivyo kuwa washindi wa jumla kwa kujikusanyia vikombe 13", alisema Dkt Chamuriho.

Hatahivyo, Dkt Chamuriho ameihimiza timu hiyo kuendelea kufanya mazoezi kwa bidii, ili kupata mafanikio makubwa Zaidi katika michezo mbalimbali.

"Siku zote kuwa namba moja sio kazi ila kazi ni kubaki namba moja, hivyo nawahimiza muendelee kufanya mazoezi ili mzidi kuleta ushindi zaidi katika mashindano mnayoshiriki", alisema Dkt Chamuriho.

Pia, Dkt Chamuriho ameahidi kushughulikia changamoto zote ambazo zimekuwa zikijitokeza mara timu hiyo inapotaka kushiriki katika mashindano mbalimbali, ikiwemo changamoto za vifaa na malipo ya fedha za kujikimu kwa wachezaji wanapoenda kushiriki katika mashindano hayo.

"Nimezisikia changamoto zote mlizozisema zote tutazifanyia kazi, lakini ni muhimu pia kuzingatia mnapokua mnapanga bajeti zenu, ili kusudi muda wote mnapohitaji kushiriki mashindano ya michezo gharama zote zinakuwa tayari zimeainishwa katika bajeti", alisema Dkt Chamuriho.

Aidha amewaasa watumishi kuzingatia weledi mara zote hasa wakati wachezaji wanaokwenda kushiriki michezo mbalimbali wanapochaguliwa na kuepusha maneno kwamba wengine wameachwa ingawa wanaviwango bora.
 
Awali Katibu Mkuu wa USC, Bw. Mbura Tenga amesema mazoezi rasmi ya kujiandaa na michezo ya SHIMIWI yataanza Agosti 28 kwenye viwanja vya michezo vya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), ambapo wachezaji watachaguliwa kupitia makocha kulingana na kuwa na viwango vya juu.

Hatahivyo Bw. Tenga amesema timu hiyo inakabiliwa na changamoto ya vifaa, posho na ruhusa za wachezaji kutoka kwenye taasisi zilizozopo chini ya Uchukuzi, na kusababisha kupeleka wachezaji wachache tofauti na matarajio ya klabu.

Naye Mkurugezi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) Bw. Paul Rwegasha ambaye alimwakilisha  Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania (TAA) Bw. Richard Mayongela amesema kwamba Mamlaka itaendelea kutoa kipaumbele katika ushiriki wake katika michezo ili kuweza kufanikisha ushindi wa pamoja katika timu.

"Napenda kukushukuru sana Katibu Mkuu kwa kuwa pamoja nasi siku hii ya leo, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini itaendelea kushiriki katika mashindano yote, ili kuonesha ushirikiano na ushikamano na kuleta ushindi wa pamoja katika sekta ya Uchukuzi", alisema Bw. Rwegasha.

Pia Mkurugezi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA),  Bw. Hamza Johari amesema kwamba Mamlaka hiyo itaendelea kupeleka wanamichezo zaidi, ili kuleta tija sehemu ya kazi, ambapo mtumishi mwenye afya njema huzalisha zaidi.

Kwa maelezo zaidi, tembelea blog yetu.

MWISHO

Contact Us

Tel (Gen): +255 22 2842402/3
Fax: +255 22 2844495
Email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
P.O.Box 18000 Dar Es Salaam

Feedback & Enquires