TAA na Kikosi Cha Zimamoto na Uokoaji Kujadili Usalama Katika Usafiri wa Anga

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imedhamiria kuleta mageuzi Makuu katika usalama wa usafiri wa Anga katika Kitengo cha Zimamoto na Uokoaji katika Viwanja 58 vilivyo chini yake vilivyo katika Mikoa mbali mbali ya Tanzania Bara.

Katika kutimiza hilo TAA leo imefanya Kikao kazi kikiongozwa na Kusimamiwa na Kamishna Jenerali wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Afande Thobias Adengenye pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bw. Lawrence Thobias na kuhudhuriwa na Makamanda wa Mikoa na Wakuu wa Vituo vya Zimamoto na Uokoaji Viwanja vya ndege Bara.

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho muhimu, Afande Kamishna Andengenye amebainisha kwamba lengo kuu la kikao kazi hicho ni kuzitambua changamoto za kiutendaji lakini pia kuboresha na kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo.

"Lengo kuu ni kuzitambua changamoto zilizopo, lakini pia kuzipatia ufumbuzi changamoto hizi hii yote itaboresha mazingira ya kazi lakini pia kuimarisha na kuendeleza mahusiano yaliyopo baina ya Mamlaka ya Viwanja Vya Ndege Tanzania (TAA) na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji" alisema Afande Andengenye.

Awali katika ufunguzi wa Kikao kazi hicho Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA Bw. Thobias amesema kwamba anatambua mchango mkubwa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika kuhakikisha kwamba Viwanja vya Ndege vinatoa huduma za Ubora wa Kimataifa.

"Mahusiano yaliyopo kati ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ni Mazuri sana na kwa sababu hiyo TAA imekua na kawaida ya kufanya baadhi ya mambo ili kuendeleza na kuimarisha mahusiano hayo,ikiwemo kutoa mafunzo kwa Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji waliopo katika Viwanja vya Ndege, mfano kwa bajeti ya mwaka 2018/19 TAA imetenga bajeti kwa ajili ya mafunzo ya askari 90 na tayari askari 30 wameshapata mafunzo kwa ajili ya kuimarisha utendaji wao.

Aidha Bw. Thobias aliongeza kwamba katika bajeti ya mwaka 2017/18 TAA ilitenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa mitambo sita ya kuzimia moto na mchakato huo upo katika hatua za mwisho kukamilika, lakini kama hiyo haitoshi pia TAA imetenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa magari ya Zimamoto lakini zaidi ya yote TAA itaendelea kuwajali Askari waliopo katika Viwanja vya Ndege kwa kutambua mchango wao mkubwa katika utoaji wa huduma bora katika Viwanja vya Ndege.

Katika hatua nyingine Mkaguzi wa Viwanja Vya Ndege kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) Bw. Burhan Hajji Majaliwa alipata fursa ya kuzungumza na kutolea ufafanuzi juu ya suala la ukaguzi ambao watu hufanyiwa katika Viwanja vya Ndege Ndege na kubainisha kwamba kila mtu anatakiwa kukaguliwa ili kuimarisha usalama katika Viwanja vya Ndege.

"Kwa mujibu wa taratibu mtu yeyote anayetumia Kiwanja cha Ndege ni lazima akaguliwe isipokua kwa viongozi wakuu wa Serikali na pia kwa watendaji wa Vikosi vya Usalama wanaweza pia wasikaguliwe wakati wa dharula" alisema Bw. Majaliwa.

Katika nafasi ya kipekee Kaimu Mkurugenzi wa Viwanja vya Ndege vya Mikoani Bw. Julius Missollow aliweza kutoa somo kwa Makamanda wa Mikoa na Wakuu wa Vituo vya Zimamoto na Uokoaji Viwanja vya ndege Bara waliohudhuria kikao kazi hicho juu ya mazoezi ya uzimaji moto wakati inapotokea dharula katika Viwanja vya Ndege.

Akitoa somo hilo Bw. Missolow alibainisha kwamba ni vyema kufanya mazoezi hayo mara kwa mara, hiyo inawafanya Askari waliopo katika Viwanja vya Ndege kuwa tayari Muda wote ili kuweza kuwaimarisha utendaji kazi wao wakati dharula inapojitokeza.

Kikao kazi hicho ni cha kwanza kufanyika baina ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na kuhudhuriwa na Kamishna Jenerali wa jeshi hilo, Mkurugenzi wa TAA na Wakuu wa Vituo vya Zimamoto na Uokoaji na ni Kikao ambacho kitakuwa endelevu kutoka sasa.

Kwa taarifa zaidi, tembelea blog yetu 

Contact Us

Tel (Gen): +255 22 2842402/3
Fax: +255 22 2844495
Email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
P.O.Box 18000 Dar Es Salaam

Feedback & Enquires