Baraza Kuu la Wafanyakazi TAA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Mhe. Isack Kamwelwe amesema Serikali ina mkakati wa kutunga sheria ya kuunganisha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)na Kampuni ya Maendeleo ya Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro (KADCO) ili kuunda Mamlaka ya usimamizi na uendeshaji wa Viwanja vya Ndege hapa nchini.

Waziri Kamwelwe alisema hayo alipokuwa akizungumza katika Mkutano wa 22 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa TAA katika Ukumbi wa LAPF Jijini Dodoma.

Aidha, Waziri Kamwelwe alisema lengo la kuunganisha TAA na KADCO ni kuwa na Mamlaka kamili ili isimamie Viwanja vya ndege na kuhudumia ndege zote pamoja na kusimamia biashara za kimkakati kama mafuta ya Ndege na utoaji huduma katika Viwanja vya Ndege.

Kamwelwe alisema "mafuta ya ndege hayadhibitiwi kama zinavyodhibitiwa nishati nyingine na EWURA. Kwa nini huku kwenye ndege msimamizi asiwepo? sasa ili kudhibiti hili mtakuwa mnauza mafuta ninyi na hii ni baada tu ya kuwa Mamlaka kamili," alihoji.

Akizungumzia Jengo la III la abiria alisema kunahitajika Watumishi zaidi ya 600 hivyo lazima Serikali iangalie wanahitajika Watumishi wa aina gani ili kuijenga TAA katika sura mpya.

Kwa upande wa ununuzi wa ndege mpya, Mhandisi Kamwelwe alisema Serikali ina mpango wa kuleta ndege mbili ambazo zitatumika kwa ajili ya mafunzo ya Urubani akitaja Kiwanja cha Ndege cha Tanga kutumiwa kwa ajili ya mafunzo hayo.

Akizungumzia viwanja vya Ndege alisema "pamoja na kuwa na viwanja 58 lakini vingi havina uzio hivyo kutokuwepo kwa uzio wa nje na uzio wa ndani kunahatarisha usalama wake 'alisema.

Awali akifungua Mkutano huo wa siku mbili Mhandisi Kamwele aliitaka TAA kuajiri watumishi kutokana na mgawanyo wa majukumu ambao unakidhi matakwa ya Taasisi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Bw. Richard Mayongela aliiomba Serikali kuijengea uwezo Taasisi ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa nyenzo za kufanyia kazi pamoja na kuajiri wafanyakazi wenye ubora.

Pia, Bw. Mayongela aliomba kuongezwa mishahara na marupurupu mengine kwa Watumishi wa Mamlaka.

"Usiwaone leo wamevaa suti lakini ukiwona siku za kawaida nyuso zao zinakosa raha kwani wana njaa," alisema

Hata hivyo alisema kuwa wakati Mamlaka inaanzishwa mwaka 1999 ilikuwa inakusanya shilingi za Kitanzania bilioni tatu hata hivyo makusanyo hayo yameweza kuongezeka mwaka hadi mwaka ambapo hadi kufikia mwaka wa fedha 2017/18 makusanyo yalikuwa ni kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 70 kwa makusanyo ya ndani.

Pamoja na Mkutano huo wa 22 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi Mamlaka ya Viwanja vya ndege leo imeweza kutimiza miaka 19 tangu kuanzishwa na kuzinduliwa kwake ambapo iliweza kuzinduliwa rasmi tarehe 3 Desemba 1999.

Baraza Kuu la Wafanyakazi hufanyika mara 2 kila mwaka kwa lengo la kujadili Taarifa za utendaji na utekelezaji za Idara na Vitengo na kujadili na kuweka maazimio mbalimbali.

Contact Us

Tel (Gen): +255 22 2842402/3
Fax: +255 22 2844495
Email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
P.O.Box 18000 Dar Es Salaam

Feedback & Enquires