JENGO LA 3 LA ABIRIA JNIA KUONGEZA CHACHU YA UCHUMI

JENGO la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII) litaongeza chachu ya kukua kwa uchumi wa nchi, imeelezwa.

Hayo yamesemwa leo na Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipozindua jengo hilo ambalo sasa limeanza kutumika kwa safari za nje ya nchi baada ya kukamilika kwake.

Rais Magufuli amesema mbali na jengo hilo litatoa ajira mbalimbali kwa wazawa, pia litaruhusu wananchi kuwekeza katika huduma mbalimbali ndani na nje ya jengo hilo, ambapo ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhakikisha Wazawa wanapewa kipaumbele katika uwekezaji katika jengo hilo.

"Serikali inaimarisha usafiri wa anga kwa kununua ndege pamoja na kuimarisha miundombinu ya viwanja vya ndege, ambapo serikali inampango wa kukarabati na kujenga viwanja 15 nchini kikiwepo cha Kimataifga cha Msalato Dodoma, ili kuendelea kuufanya usafiri huu uendelee kuwa wa haraka na salama, ambapo utachangia kukuza pato la taifa kwa watumiaji wake, ambao kwa sasa abiria wameongezeka kwa asilimia 12 kwa mwaka," amesema Mhe. Rais.

Amesema anaimani idadi ya abiria wa ndege wataongezeka zaidi kutokana na utalii unakwenca sambamba na usafiri wa anga, kutokana na Watalii wengi huja nchini kwa kutumia usafiri wa anga.

Hatahivyo, ameipongeza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kwa kufanikisha kukamilika kwa mradi huo mkubwa wa jengo hilo, ambao mwaka 2016 ulisuasua kutokana na kukosekana kwa fedha za kuendelea na mradi.

Amewataka Watanzania kulipa kodi ili serikali iweze kukamilisha mapema kwa wakati miradi mikubwa, ambayo itakuja kuwanufaisha na kuwapa heshima kubwa.

"Miradi inawezekana kwani fedha nyingi zilikuwa zikitumiwa na mafisadi, hivyo nawataka tulipe kodi ili kufanikisha miradi yote, na tuachane na dhana ya wafadhili ambao wamekuwa na masharti," amesema Mhe. Rais.

Hatahivyo, amewataka watumiaji wote wa Jengo hili kuhakikisha wanalitunza na wasiliharibu kutokana na kujengwa kwa fedha nyingi za Watanzania.

Katika hatua nyingine amempongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Kikwete aliyeanzisha ujenzi wa mradi wa Jengo la Tatu la abiria, na pia amewashukuru viongozi wa Dini nchini kuendelea kuliombea taifa.

Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kutokana na ongezeko la mara kwa mara la abiria, sasa Jengo la pili la abiria (JNIA-TBII) linaboreshwa na kukarabatiwa ili liweze kuhudumia abiria mara mbili ya sasa ambao ni Milioni 1.5 kwa mwaka.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patric Mfugale, ambao ndio walikuwa wasimamizi wa mradi huu wa kimkakati amesema jengo hili limekuja wakati muafaka kutokana na wananchi kuwa na mwamko wa kupanda ndege, ambapo kumekuwa na ongezeko la abiria, ambapo kwa sasa kati ya ndege 23 za nje tayari 18 zimeanza kutumia jengo hili.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi Julius Ndyamukama amesema TAA wapo tayari kuendesha huduma kwenye jengo hilo, ambapo wamefanya majaribio kadhaa ya ndege, ambapo tarehe 17 Julai, 2019 walianza na ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), iliyokuwa ikizindua safari yake ya kwanza kwenda nchini India.

Kwa upande wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai amesema jengo hili la kisasa linaitoa Tanzania kimasomaso, kutokana na ukubwa na ubora wake.

"Nipo hapa kuwawakilisha Wabunge, ambapo tunaona fedha tunazopitisha zinatumika kihalali na tutaendelea kumuunga mkono Mhe. Rais katika jitihada zake za kuendeleza na kuanzisha miradi mbalimbali," amesema Mhe. Spika.

Naye Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma ame wataka wananchi kuhakikisha wanatatua migogoro yao ya ardhi inayohusisha ujenzi wa miradi mbalimbali nje ya mahakama, ili kufanikisha miradi hiyo kumalizika kwa wakati.

Contact Us

Tel (Gen): +255 22 2842402/3
Fax: +255 22 2844495
Email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
P.O.Box 18000 Dar Es Salaam

Feedback & Enquires